5. Angalieni nimewafundisha amri na hukumu, vile vile kama BWANA, Mungu wangu, alivyoniamuru, ili mzitende katika nchi mwingiayo ili kuimiliki.
6. Zishikeni basi, mkazitende, maana hii ndiyo hekima yenu na akili zenu, machoni pa mataifa watakaozisikia amri hizi zote, nao watasema, Hakika taifa hili kubwa ni watu wenye hekima na akili.
7. Kwa maana liko taifa gani kubwa, lililo na Mungu aliye karibu nao, kama BWANA, Mungu wetu, alivyo, kila tumwitapo?
8. Tena liko taifa gani kubwa, lililo na amri na hukumu zenye haki kama torati hii yote, ninayoiweka mbele yenu leo.
9. Lakini, jihadhari nafsi yako, ukailinde roho yako kwa bidii, usije ukayasahau mambo yale uliyoyaona kwa macho yako, yakaondoka moyoni mwako siku zote za maisha yako; bali uwajulishe watoto wako na watoto wa watoto wako;
10. siku ile uliyosimama mbele za BWANA wako huko Horebu, BWANA aliponiambia, Nikusanyieni watu hawa, nami nitawasikizisha maneno yangu, ili wajifunze kunicha mimi siku zote watakazoishi duniani, wakapate na kuwafundisha watoto wao.
11. Mkakaribia, mkasimama chini ya ule mlima; mlima ukawaka moto mpaka kati ya mbinguni, kwa giza na mawingu, na giza kuu.
12. BWANA akasema nanyi kutoka kati ya moto; mkasikia sauti ya maneno, lakini hamkuona umbo lo lote; sauti tu.
13. Akawahubiri agano lake, alilowaamuru kulitenda, yaani, zile amri kumi; akaziandika juu ya mbao mbili za mawe.
14. BWANA akaniamuru wakati ule niwafundishe maagizo na hukumu, mpate kuzitenda katika nchi ile mtakayoivukia ili kuimiliki.
15. Jihadharini nafsi zenu basi; maana hamkuona umbo la namna yo yote siku ile BWANA aliyosema nanyi kutoka kati ya moto;
16. msije mkajiharibu nafsi zenu, mkajifanyia sanamu ya kuchonga, mfano wa sura yo yote, mfano wa mwanamume au mwanamke,
17. mfano wa mnyama ye yote aliye duniani, au mfano wa ndege ye yote arukaye mbinguni,
18. au mfano wa kitu cho chote kitambaacho juu ya ardhi, au mfano wa samaki ye yote aliye majini chini ya nchi;
19. tena usije ukainua macho yako hata mbinguni, na ulionapo jua, na mwezi, na nyota, jeshi la mbinguni lote pia, ukashawishwa na kuviabudu, na kuvitumikia, ambavyo BWANA, Mungu wako amewagawanyia watu wote chini ya mbingu zote.
20. Bali BWANA amewatwaa ninyi, na kuwatoa katika tanuu ya chuma, katika Misri, mpate kuwa watu wa urithi kwake, kama mlivyo leo hivi.
21. Tena BWANA alinikasirikia kwa ajili yenu, akaapa ya kwamba sitavuka Yordani, na ya kwamba sitaingia nchi ile njema, awapayo BWANA, Mungu wenu, iwe urithi.