40. Basi, zishike sheria zake, na amri zake, ninazokuamuru leo, upate kufanikiwa, wewe na watoto wako baada yako, na siku zako ziwe nyingi katika nchi ile akupayo BWANA, Mungu wako, milele.
41. Ndipo Musa akabagua miji mitatu ng’ambo ya Yordani upande wa matokeo ya jua;
42. ili kwamba amwuaye mtu apate kukimbilia huko, amwuaye jirani yake pasipo kujua, wala hakumchukia tangu hapo; ili apate kuishi akimbiliapo mmojawapo miji hiyo;
43. nayo ni hii, Beseri ya barani iliyo katika nchi tambarare, kwa Wareubeni; na Ramothi iliyo Gileadi, kwa Wagadi; na Golani iliyo Bashani, kwa Wamanase.
44. Na torati Musa aliyowawekea wana wa Israeli ni hii;
45. haya ndiyo mashuhudizo, na amri, na hukumu, Musa alizowaambia wana wa Israeli walipotoka Misri;
46. ng’ambo ya Yordani, katika bonde lililoelekea Beth-peori, katika nchi ya Sihoni mfalme wa Waamori, aliyekuwa akikaa Heshboni ndiye aliyepigwa na Musa na wana wa Israeli, walipotoka Misri;
47. wakaishika nchi yake, ikawa milki yao, na nchi ya Ogu mfalme wa Bashani, ndio wafalme wawili wa Waamori, waliokuwa ng’ambo ya Yordani upande wa matokeo ya jua;