Kum. 4:24-35 Swahili Union Version (SUV)

24. kwa kuwa BWANA, Mungu wenu, ni moto ulao, Mungu mwenye wivu.

25. Utakapozaa wana, na wana wa wana, mkisha kuwa katika nchi siku nyingi, mkajiharibu na kufanya sanamu ya kuchonga kwa umbo la kitu cho chote, mkafanya ambayo ni maovu machoni pa BWANA, Mungu wako, na kumtia hasira;

26. nawashuhudizia mbingu na nchi hivi leo, kwamba karibu mtaangamia kabisa juu ya nchi mwivukiayo Yordani kuimiliki, hamtafanya siku zenu ziwe nyingi juu yake, ila mtaangamizwa kabisa.

27. Na BWANA atawatawanya kati ya mataifa, nanyi mtasalia watu kidogo hesabu yenu kati ya makabila, mtakakopelekwa mbali na BWANA.

28. Na huko mtatumikia miungu, kazi za mikono ya watu, miti na mawe, ambao hawaoni, wala hawasikii, hawali, wala hawanusi.

29. Lakini huko, kama mkimtafuta BWANA, Mungu wako, utampata, ukimtafuta kwa moyo wako wote, na roho yako yote.

30. Na wakati uwapo katika mashaka, ukiisha kupatwa na mambo haya yote, siku za mwisho, utamrudia BWANA, Mungu wako, na kuisikiza sauti yake;

31. kwa kuwa BWANA, Mungu wako, ni Mungu wa rehema; hatakukosa wala kukuangamiza, wala hatalisahau agano la baba zako alilowaapia.

32. Maana uliza sasa siku zilizopita, zilizokuwa kabla yako, tangu siku ile Mungu aliyoumba mwanadamu juu ya nchi, na toka pembe hii ya mbingu hata pembe hii, kwamba kumetukia neno lo lote kama neno hili kubwa, au kwamba kumesikiwa habari ya neno kama hili?

33. Je! Watu wakati wo wote wameisikia sauti ya Mungu ikinena toka kati ya moto, kama wewe ulivyosikia, wasife?

34. Au Mungu amekwenda wakati gani akajitwalia taifa toka kati ya taifa lingine, kwa majaribu, na kwa ishara, na kwa maajabu, na kwa vita, na kwa mkono hodari, na kwa mkono ulionyoshwa, na kwa maogofya makuu, kama vile BWANA, Mungu wenu, alivyowatendea ninyi katika Misri, mbele ya macho yenu?

35. Wewe umeonyeshwa haya, ili upate kujua ya kuwa BWANA ndiye Mungu, hapana mwingine ila yeye.

Kum. 4