22. Lakini mimi nitakufa katika nchi hii, sina ruhusa kuvuka Yordani; bali ninyi mtavuka, na kuimiliki nchi ile njema.
23. Jihadharini nafsi zenu, msije mkalisahau agano la BWANA, Mungu wenu, alilolifanya nanyi, mkajifanyia sanamu ya kuchonga, mfano wa umbo la kitu cho chote ulichokatazwa na BWANA, Mungu wenu,
24. kwa kuwa BWANA, Mungu wenu, ni moto ulao, Mungu mwenye wivu.
25. Utakapozaa wana, na wana wa wana, mkisha kuwa katika nchi siku nyingi, mkajiharibu na kufanya sanamu ya kuchonga kwa umbo la kitu cho chote, mkafanya ambayo ni maovu machoni pa BWANA, Mungu wako, na kumtia hasira;
26. nawashuhudizia mbingu na nchi hivi leo, kwamba karibu mtaangamia kabisa juu ya nchi mwivukiayo Yordani kuimiliki, hamtafanya siku zenu ziwe nyingi juu yake, ila mtaangamizwa kabisa.
27. Na BWANA atawatawanya kati ya mataifa, nanyi mtasalia watu kidogo hesabu yenu kati ya makabila, mtakakopelekwa mbali na BWANA.