Kum. 4:12-24 Swahili Union Version (SUV)

12. BWANA akasema nanyi kutoka kati ya moto; mkasikia sauti ya maneno, lakini hamkuona umbo lo lote; sauti tu.

13. Akawahubiri agano lake, alilowaamuru kulitenda, yaani, zile amri kumi; akaziandika juu ya mbao mbili za mawe.

14. BWANA akaniamuru wakati ule niwafundishe maagizo na hukumu, mpate kuzitenda katika nchi ile mtakayoivukia ili kuimiliki.

15. Jihadharini nafsi zenu basi; maana hamkuona umbo la namna yo yote siku ile BWANA aliyosema nanyi kutoka kati ya moto;

16. msije mkajiharibu nafsi zenu, mkajifanyia sanamu ya kuchonga, mfano wa sura yo yote, mfano wa mwanamume au mwanamke,

17. mfano wa mnyama ye yote aliye duniani, au mfano wa ndege ye yote arukaye mbinguni,

18. au mfano wa kitu cho chote kitambaacho juu ya ardhi, au mfano wa samaki ye yote aliye majini chini ya nchi;

19. tena usije ukainua macho yako hata mbinguni, na ulionapo jua, na mwezi, na nyota, jeshi la mbinguni lote pia, ukashawishwa na kuviabudu, na kuvitumikia, ambavyo BWANA, Mungu wako amewagawanyia watu wote chini ya mbingu zote.

20. Bali BWANA amewatwaa ninyi, na kuwatoa katika tanuu ya chuma, katika Misri, mpate kuwa watu wa urithi kwake, kama mlivyo leo hivi.

21. Tena BWANA alinikasirikia kwa ajili yenu, akaapa ya kwamba sitavuka Yordani, na ya kwamba sitaingia nchi ile njema, awapayo BWANA, Mungu wenu, iwe urithi.

22. Lakini mimi nitakufa katika nchi hii, sina ruhusa kuvuka Yordani; bali ninyi mtavuka, na kuimiliki nchi ile njema.

23. Jihadharini nafsi zenu, msije mkalisahau agano la BWANA, Mungu wenu, alilolifanya nanyi, mkajifanyia sanamu ya kuchonga, mfano wa umbo la kitu cho chote ulichokatazwa na BWANA, Mungu wenu,

24. kwa kuwa BWANA, Mungu wenu, ni moto ulao, Mungu mwenye wivu.

Kum. 4