23. Nitaweka madhara juu yao chunguchungu;Nitawapiga kwa mishale yangu hata ikaishe;
24. Watakonda kwa njaa, wataliwa na makaa ya moto,Na uharibifu mkali;Nitawapelekea meno ya wanyama wakali,Pamoja na sumu ya wadudu watambaao mavumbini.
25. Nje upanga utawafifilizaNa ndani ya vyumba, utisho;Utaangamiza mvulana na msichana,Anyonyaye pamoja na mwenye mvi,
26. Nalisema, Ningewatawanyia mbali,Ningekomesha kumbukumbu lao kati ya wanadamu;
27. Isipokuwa naliogopa makamio ya adui,Adui zao wasije wakafikiri uongo,Wasije wakasema, Mkono wetu umetukuka,Wala BWANA hakuyafanya haya yote.
28. Maana hawa ni taifa wasio shauri,Wala fahamu hamna ndani yao.
29. Laiti wangekuwa na akili, hata wakafahamu haya,Ili watafakari mwisho wao.
30. Mmoja angefukuzaje watu elfu,Wawili wangekimbizaje elfu kumi,Kama Mwamba wao asingaliwauza,Kama BWANA asingaliwatoa?
31. Maana, Mwamba wao si kama Mwamba wetu,Hata adui zetu wenyewe ndivyo wahukumuvyo.
32. Maana, mzabibu wao ni mzabibu wa Sodoma,Nao ni wa mashamba ya Gomora;Zabibu zao ni zabibu za uchungu,Vichala vyao ni vichungu.