Kum. 31:17-30 Swahili Union Version (SUV)

17. Ndipo hasira yangu itakapowaka juu yao siku hiyo, nami nitawaacha, nitawaficha uso wangu, nao wataliwa, tena watajiliwa na mambo maovu mengi na mashaka; hata waseme siku hiyo, Je! Kujiliwa kwetu na maovu haya si kwa sababu Mungu wetu hayumo kati yetu?

18. Nami nitawaficha uso wangu kwa kweli siku hiyo, kwa maovu yote waliyoyafanya, kwa kuigeukia hiyo miungu mingine.

19. Basi sasa jiandikieni wimbo huu, uwafundishe wana wa Israeli; kawatie vinywani mwao, ili uwe shahidi kwangu wimbo huu, juu ya wana wa Israeli.

20. Kwa kuwa nitakapokwisha kuwatia katika nchi niliyowaapia baba zao, imiminikayo maziwa na asali; nao watakapokwisha kula na kushiba, na kuwanda; ndipo watakapoigeukia hiyo miungu mingine, na kuitumikia, na kunidharau mimi, na kulivunja agano langu.

21. Tena itakuwa, wakiisha kujiliwa na mambo maovu mengi na mashaka, utashuhudia wimbo huu mbele yao kama shahidi, kwa maana hautasahauliwa katika vinywa vya uzao wao; kwani nayajua mawazo yao wayawazayo, hata sasa kabla sijawatia katika nchi niliyoapa.

22. Basi Musa akauandika wimbo huu siku iyo hiyo, akawafundisha wana wa Israeli.

23. Akamwagiza Yoshua, mwana wa Nuni, akamwambia, Uwe hodari na moyo mkuu, kwa kuwa utawapeleka wana wa Israeli katika nchi niliyowaapia; nami nitakuwa pamoja nawe.

24. Basi ikawa hapo Musa alipomaliza kuandika maneno ya torati hii katika chuo, hata yakaisha,

25. ndipo Musa akawaamuru Walawi waliokuwa wakilichukua sanduku la agano la BWANA akawaambia,

26. Twaeni chuo hiki cha torati, mkiweke kando ya sanduku la agano la BWANA, Mungu wenu, ili kiwepo kama shahidi juu yako.

27. Kwa kuwa uasi wako naujua, na shingo yako ngumu; angalieni, mimi nikali hai pamoja nanyi leo, mmekuwa waasi juu ya BWANA; siuze nitakapokwisha kufa!

28. Nikutanishieni wazee wote wa kabila zenu, na maakida yenu, ili niseme maneno haya masikioni mwao, na kuwashuhudizia mbingu na nchi juu yao.

29. Kwa sababu najua baada ya kufa kwangu mtajiharibu kabisa, na kukengeuka katika njia niliyowaamuru; nayo mabaya yatawapata siku za mwisho, kwa vile mtakavyofanya maovu machoni pa BWANA kumtia kasirani kwa kazi ya mikono yenu.

30. Musa akasema maneno ya wimbo huu masikioni mwa kusanyiko la wana wa Israeli hata yakaisha.

Kum. 31