Kum. 30:7-16 Swahili Union Version (SUV)

7. Na laana hizi zote BWANA, Mungu wako, atawatia adui zako na hao wakuchukiao, waliokuwa wakikutesa.

8. Nawe utarudi, uitii sauti ya BWANA, na kuyafanya maagizo yake yote nikuagizayo leo.

9. Na BWANA, Mungu wako, atakufanya uwe na wingi wa uheri katika kazi yote ya mkono wako, katika uzao wa tumbo lako, na katika uzao wa ng’ombe wako, na katika uzao wa nchi yako; kwa kuwa BWANA atafurahi tena juu yako kwa wema, kama alivyofurahi juu ya baba zako;

10. ukiwa utaifuata sauti ya BWANA, Mungu wako, kwa kuyashika maagizo yake, na amri zake zilizoandikwa katika chuo hiki cha torati; ukimwelekea BWANA, Mungu wako, kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote.

11. Kwa maana maagizo haya nikuagizayo leo, si mazito mno kwako, wala si mbali.

12. Si mbinguni, hata useme, Ni nani atakayetupandia mbinguni akatuletee, aje atuambie tusikie, tupate kuyafanya?

13. Wala si ng’ambo ya pili ya bahari, hata useme, Ni nani atakayetuvukia bahari, akatuletee, aje atuambie, tusikie, tupate kuyafanya?

14. Lakini neno li karibu nawe sana, li katika kinywa chako na moyo wako, upate kulifanya.

15. Angalia, nimekuwekea leo mbele yako uzima na mema, na mauti na mabaya;

16. kwa hivi nikuagizavyo leo kumpenda BWANA, Mungu wako, kuenenda katika njia zake, na kushika maagizo yake, na amri zake, na hukumu zake, upate kuwa hai na kuongezeka; BWANA, Mungu wako, apate kukubarikia katika nchi uingiayo kuimiliki.

Kum. 30