Kum. 30:10-20 Swahili Union Version (SUV)

10. ukiwa utaifuata sauti ya BWANA, Mungu wako, kwa kuyashika maagizo yake, na amri zake zilizoandikwa katika chuo hiki cha torati; ukimwelekea BWANA, Mungu wako, kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote.

11. Kwa maana maagizo haya nikuagizayo leo, si mazito mno kwako, wala si mbali.

12. Si mbinguni, hata useme, Ni nani atakayetupandia mbinguni akatuletee, aje atuambie tusikie, tupate kuyafanya?

13. Wala si ng’ambo ya pili ya bahari, hata useme, Ni nani atakayetuvukia bahari, akatuletee, aje atuambie, tusikie, tupate kuyafanya?

14. Lakini neno li karibu nawe sana, li katika kinywa chako na moyo wako, upate kulifanya.

15. Angalia, nimekuwekea leo mbele yako uzima na mema, na mauti na mabaya;

16. kwa hivi nikuagizavyo leo kumpenda BWANA, Mungu wako, kuenenda katika njia zake, na kushika maagizo yake, na amri zake, na hukumu zake, upate kuwa hai na kuongezeka; BWANA, Mungu wako, apate kukubarikia katika nchi uingiayo kuimiliki.

17. Lakini moyo wako ukikengeuka, usipotaka kusikiza, lakini ukavutwa kando kwenda kuabudu miungu mingine, na kuitumikia;

18. nawahubiri hivi leo hakika mtaangamia; hamtazifanya siku zenu kuwa nyingi juu ya nchi, uivukiayo Yordani, uingie kuimiliki.

19. Nazishuhudiza mbingu na nchi juu yenu hivi leo, kuwa nimekuwekea mbele yako uzima na mauti, baraka na laana; basi chagua uzima, ili uwe hai, wewe na uzao wako;

20. kumpenda BWANA, Mungu wako, kuitii sauti yake, na kushikamana naye; kwani hiyo ndiyo uzima wako, na wingi wa siku zako; upate kukaa katika nchi BWANA aliyowaapia baba zako, Ibrahimu, na Isaka, na Yakobo, kuwa atawapa.

Kum. 30