20. hata BWANA awapumzishe ndugu zenu kama ninyi, nao pia waimiliki nchi wapewayo na BWANA, Mungu wenu, ng’ambo ya Yordani; ndipo mtakaporudi kila mmoja aende katika milki yake niliyowapa.
21. Nikamwamuru Yoshua wakati huo, nikamwambia, Macho yako yameona yote aliyowatenda BWANA, Mungu wenu, wale wafalme wawili, navyo ndivyo atakavyoutenda BWANA kila ufalme huko uvukiako.
22. Msiwache, kwa kuwa BWANA, Mungu wenu, ndiye awapiganiaye.
23. Nikamnyenyekea BWANA wakati huo, nikamwambia,
24. Ee BWANA Mungu, umeanza kumwonyesha mtumishi wako ukubwa wako, na mkono wako wa nguvu; kwani kuna mungu gani mbinguni au duniani awezaye kufanya mfano wa kazi zako, na mfano wa matendo yako yenye nguvu?
25. Nami nakuomba nivuke, nikaione hiyo nchi nzuri iliyoko ng’ambo ya Jordani, mlima ule mzuri, na Lebanoni.
26. Lakini BWANA alikuwa amenikasirikia kwa ajili yenu, asinisikize; BWANA akaniambia, Na ikutoshe, usinene nami zaidi jambo hili.
27. Kwea katika kilele cha Pisga ukainue macho yako upande wa magharibi, na kaskazini, na kusini, na mashariki, ukatazame kwa macho yako, kwa maana huuvuki mto huu wa Yordani.
28. Lakini mwagize Yoshua umtie moyo mkuu, umtie na nguvu; kwani ndiye atakayevuka mbele ya watu hawa, na nchi utakayoiona atawarithisha yeye.
29. Basi tukakaa katika bonde lililoelekea Beth-peori.