Kum. 3:14-29 Swahili Union Version (SUV)

14. Yairi, mwana wa Manase, alitwaa nchi yote ya Argobu, hata mpaka wa Wageshuri na Wamaaka; akaziita nchi hizo Hawoth-yairi, kwa jina lake mwenyewe, hata hivi leo, maana, hizo nchi za Bashani.)

15. Na Makiri nilimpa Gileadi.

16. Na Wareubeni na Wagadi niliwapa tokea Gileadi mpaka bonde la Arnoni, katikati ya bonde, na mpaka wake; mpaka mto wa Yaboki, nao ni mpaka wa wana wa Amoni;

17. na nchi ya Araba nayo, na mto wa Yordani, na mpaka wake, tokea Kinerethi mpaka bahari ya hiyo Araba, nayo ni Bahari ya Chumvi, chini ya matelemko ya Pisga, upande wa mashariki.

18. Nikawaamuru wakati huo, nikawaambia, BWANA, Mungu wenu, amewapa ninyi nchi hii mwimiliki, basi vukeni ng’ambo wenye silaha mbele ya ndugu zenu, wana wa Israeli, nyote mlio mashujaa.

19. Lakini wake wenu na watoto wenu, na wanyama wenu wa mji, (nawajua kwamba mna wanyama wengi), na wakae katika miji yenu niliyowapa;

20. hata BWANA awapumzishe ndugu zenu kama ninyi, nao pia waimiliki nchi wapewayo na BWANA, Mungu wenu, ng’ambo ya Yordani; ndipo mtakaporudi kila mmoja aende katika milki yake niliyowapa.

21. Nikamwamuru Yoshua wakati huo, nikamwambia, Macho yako yameona yote aliyowatenda BWANA, Mungu wenu, wale wafalme wawili, navyo ndivyo atakavyoutenda BWANA kila ufalme huko uvukiako.

22. Msiwache, kwa kuwa BWANA, Mungu wenu, ndiye awapiganiaye.

23. Nikamnyenyekea BWANA wakati huo, nikamwambia,

24. Ee BWANA Mungu, umeanza kumwonyesha mtumishi wako ukubwa wako, na mkono wako wa nguvu; kwani kuna mungu gani mbinguni au duniani awezaye kufanya mfano wa kazi zako, na mfano wa matendo yako yenye nguvu?

25. Nami nakuomba nivuke, nikaione hiyo nchi nzuri iliyoko ng’ambo ya Jordani, mlima ule mzuri, na Lebanoni.

26. Lakini BWANA alikuwa amenikasirikia kwa ajili yenu, asinisikize; BWANA akaniambia, Na ikutoshe, usinene nami zaidi jambo hili.

27. Kwea katika kilele cha Pisga ukainue macho yako upande wa magharibi, na kaskazini, na kusini, na mashariki, ukatazame kwa macho yako, kwa maana huuvuki mto huu wa Yordani.

28. Lakini mwagize Yoshua umtie moyo mkuu, umtie na nguvu; kwani ndiye atakayevuka mbele ya watu hawa, na nchi utakayoiona atawarithisha yeye.

29. Basi tukakaa katika bonde lililoelekea Beth-peori.

Kum. 3