Kum. 29:6-18 Swahili Union Version (SUV)

6. Hamkula mkate, wala hamkunywa divai, wala kileo; ili mpate kujua kwamba Mimi ndimi BWANA, Mungu wenu.

7. Nanyi mlipokuja mahali hapa, walitutokea kupigana juu yetu Sihoni mfalme wa Heshboni, na Ogu mfalme wa Bashani, tukawapiga;

8. tukaitwaa nchi yao, nayo tukawapa Wareubeni, na Wagadi, na nusu ya kabila ya Manase, iwe urithi.

9. Shikeni basi maneno ya agano hili myafanye, ili mfanikiwe katika yote mfanyayo.

10. Leo mmesimama nyote mbele za BWANA, Mungu wenu; wakuu wenu, na kabila zenu, na wazee wenu, na maakida wenu, waume wote wa Israeli,

11. vijana vyenu, na wake wenu, na mgeni wako aliye kati ya kituo chako, tokea mchanjaji wa kuni zako hata mtekaji wa maji yako;

12. ili uingie katika agano la BWANA, Mungu wako, na kiapo chake, afanyacho nawe BWANA, Mungu wako, hivi leo;

13. apate kukuweka leo uwe taifa kwake naye apate kuwa Mungu kwako, kama alivyokuambia, na kama alivyowaapia baba zako, Ibrahimu, na Isaka, na Yakobo.

14. Wala sifanyi na ninyi peke yenu agano hili na kiapo hiki;

15. ila na yeye aliyesimama hapa nasi hivi leo mbele ya BWANA, Mungu wetu, na yeye naye asiyekuwapo pamoja nasi leo;

16. (kwani mwajua mlivyoketi nchi ya Misri, na tulivyo kuja katikati ya mataifa hayo mliyopita katikati yao;

17. nanyi mliona machukizo yao, na sanamu zao, miti na mawe, fedha na dhahabu, zilizokuwako kwao;)

18. asiwe mtu katikati yenu, mume wala mke, wala jamaa, wala kabila, ageukaye moyo wake leo amwache BWANA, Mungu wetu, kwenda kuitumikia miungu ya mataifa hayo; lisiwe katikati yenu shina lizaalo uchungu na pakanga;

Kum. 29