30. Utaposa mke na mume mwingine atalala naye; utajenga nyumba usiikae; utapanda mizabibu usitumie matunda yake.
31. Ng’ombe wako atachinjwa mbele ya macho yako, usile nyama yake; utanyang’anywa punda wako mbele ya uso wako kwa jeuri, usirudishiwe; kondoo zako watapewa adui zako, usipate mtu wa kukuokoa.
32. Wanao na binti zako litapewa taifa lingine, na macho yako yataangalia, na kuzimia kwa kuwatamani mchana kutwa; wala hapatakuwa na kitu katika uwezo wa mkono wako.
33. Matunda ya nchi yako, na taabu yako yote, vitaliwa na taifa usilolijua; utaonewa tu, na kupondwa chini daima;
34. hata uwe mwenye wazimu kwa yaonwayo na macho yako, utakayoyaona.
35. BWANA atakupiga magoti na miguu kwa jipu lililo zito, usilopata kupozwa, tokea wayo wa mguu mpaka utosi wa kichwa.
36. BWANA atakupeleka wewe, na mfalme wako utakayemweka juu yako, kwa taifa usilolijua wewe wala baba zako; nawe huko utatumikia miungu mingine ya miti na mawe.
37. Nawe utakuwa ushangao, na mithali, na dharau, kati ya mataifa yote huko atakakokuongoza BWANA.
38. Mbegu nyingi utazichukua nje shambani, lakini utavuna haba, kwa kuwa nzige watazila.
39. Utapanda mizabibu na kuitengeza, wala hutakunywa katika divai yake, wala kuichuma kwani italiwa na mabuu.