Kum. 28:3-18 Swahili Union Version (SUV)

3. Utabarikiwa mjini, utabarikiwa na mashambani.

4. Utabarikiwa uzao wa tumbo lako, na uzao wa nchi yako, na uzao wa wanyama wako wa mifugo, maongeo ya ng’ombe wako, na wadogo wa kondoo zako.

5. Litabarikiwa kapu lako, na chombo chako cha kukandia unga.

6. Utabarikiwa uingiapo, utabarikiwa na utokapo.

7. BWANA atawafanya adui zako wainukao juu yako kupigwa mbele yako; watakutokea kwa njia moja, lakini watakimbia mbele yako kwa njia saba.

8. BWANA ataiamuru baraka ije juu yako katika ghala zako, na mambo yote utakayotia mkono wako; naye atakubarikia katika nchi akupayo BWANA, Mungu wako.

9. BWANA atakuweka uwe taifa takatifu kwake, kama alivyokuapia; utakaposhika maagizo ya BWANA, Mungu wako, na kutembea katika njia zake.

10. Na mataifa yote ya duniani watakuona umeitwa kwa jina la BWANA, nao watakuwa na hofu kwako.

11. BWANA atakufanya uwe na wingi wa uheri, katika uzao wa tumbo lako, na uzao wa wanyama wako wa mifugo, na uzao wa nchi yako, katika nchi BWANA aliyowaapia baba zako kwamba atakupa.

12. Atakufunulia BWANA hazina yake nzuri, nayo ni mbingu, kwa kutoa mvua ya nchi yako kwa wakati wake, na kwa kubarikia kazi yote ya mkono wako; nawe utakopesha mataifa mengi, wala hutakopa wewe.

13. BWANA atakufanya kuwa kichwa, wala si mkia; nawe utakuwa juu tu, wala huwi chini; utakapoyasikiza maagizo ya BWANA, Mungu wako, nikuagizayo hivi leo, kuyaangalia na kufanya;

14. msipokengeuka katika maneno niwaamuruyo leo kwa lo lote, kwenda mkono wa kuume wala wa kushoto, kwa kuifuata miungu mingine na kuitumikia.

15. Lakini itakuwa usipotaka kuisikiza sauti ya BWANA, Mungu wako, usiyaangalie kufanya maagizo yake yote na amri zake, nikuagizazo hivi leo, ndipo zitakapokujia laana hizi zote na kukupata.

16. Utalaaniwa mjini, utalaaniwa na mashambani.

17. Litalaaniwa kapu lako na chombo chako cha kukandia.

18. Utalaaniwa uzao wa tumbo lako, na uzao wa nchi yako, maongeo ya ng’ombe wako, na wadogo wa kondoo zako.

Kum. 28