7. Ni mtu gani aliye hapa aliyemposa mke wala hajaoa? Aende akarudi nyumbani kwake asije akafa mapiganoni, huyo mwanamke akaolewa na mume mwingine.
8. Tena maakida na waseme zaidi na watu, wawaambie, Ni mtu gani aliye hapa tena mwenye hofu na moyo mnyonge? Aende akarudi nyumbani kwake, isije mioyo ya nduguze ikayeyuka mfano wa moyo wake.
9. Itakuwa hapo watakapokwisha wale maakida kusema na watu, na waweke majemadari wa majeshi juu ya watu.
10. Utakaposongea karibu ya mji kwenda kupigana juu yake, ndipo utakapowapigia ukelele wa amani.
11. Itakuwa utakapokujibu kwa amani, na kukufungulia, ndipo watu wote watakaoonekana humo watakufanyia kazi ya shokoa, na kukutumikia.
12. Na kwamba hautaki kufanya amani nawe, lakini utafanya vita juu yako, ndipo uuhusuru;
13. na BWANA, Mungu wako, autiapo mkononi mwako, mpige kila mume aliyemo kwa makali ya upanga;
14. lakini wanawake na watoto, na wanyama wa miji, na vilivyo mjini vyote, navyo ni nyara zake zote, uvitwae viwe mateka kwako; nawe utakula nyara za adui zako alizokupa BWANA, Mungu wako.
15. Utaifanyia vivyo miji yote iliyo mbali sana nawe, isiyokuwa miji ya mataifa haya.
16. Lakini katika miji ya mataifa haya akupayo BWANA, Mungu wako, kuwa urithi, usihifadhi kuwa hai kitu cho chote kipumzikacho;
17. lakini uwaangamize kabisa, Mhiti, na Mwamori, na Mkanaani, na Mperizi, na Mhivi, na Myebusi, kama alivyokuamuru BWANA, Mungu wako;
18. wasije wakawafunza kufanya mfano wa machukizo yao yote, waliyoifanyia miungu yao; hivyo itakuwa ni makosa juu ya BWANA, Mungu wenu.
19. Wewe utakapohusuru mji siku nyingi kwa kufanya vita juu yake, upate kuutwaa, usiangamize miti yake kwa kupeleka shoka juu yake, kwani utaweza kula matunda yake; wala usiiteme, kwa maana huo mti wa kondeni, je! Ni mtu, hata ukauzuie?
20. Ila miti uijuayo si miti ya kuliwa iangamize, na kuitema; ukajenge maburuji juu ya mji ufanyao vita juu yako, hata uanguke.