18. Hivi leo ivuke Ari, mpaka wa Moabu;
19. na utakaposongea kuwaelekea wana wa Amoni, usiwasumbue wana wa Amoni, wala usishindane nao; kwa kuwa sitakupa katika nchi ya hao wana wa Amoni kuwa milki yako; kwa sababu nimewapa wana wa Lutu iwe milki yao.
20. (Nchi hiyo nayo yadhaniwa kuwa ni nchi ya Warefai, hapo kale Warefai walikaa humo; lakini Waamoni huwaita Wazamzumi;
21. nao ni watu wengi, wakubwa, warefu, kama Waanaki; lakini BWANA aliwaangamiza mbele yao; wakawafuata wakakaa badala yao;
22. kama vile alivyowafanyia wana wa Esau, waliokaa Seiri, alipowaangamiza Wahori mbele yao; wakawafuata, wakakaa badala yao hata hivi leo;
23. na Waavi waliokuwa wakikaa katika vijiji mpaka Gaza waliangamizwa na Wakaftori waliotoka Kaftori, na hawa wakakaa badala yao.)
24. Ondokeni, mshike safari yenu, mvuke bonde la Arnoni; tazama, nimemtia Sihoni Mwamori mfalme wa Heshboni mkononi mwako, na nchi yake; anzeni kuimiliki, mshindane naye katika mapigano.
25. Hivi leo nitaanza mimi kutia utisho wako na kuhofiwa kwako juu ya watu walio chini ya mbingu kila mahali, watakaosikia uvumi wako, na kutetemeka, na kuingiwa na uchungu kwa sababu yako.
26. Nikatuma wajumbe kutoka bara ya Kedemothi kwenda kwa Sihoni mfalme wa Heshboni na maneno ya amani, kusema.
27. Nipishe katikati ya nchi yako; nitakwenda kwa njia ya barabara, sitageuka kwenda mkono wa kuume wala wa kushoto.
28. Nawe uniuzie chakula kwa fedha nile; unipe na maji kwa fedha, ninywe; ila unipishe katikati kwa miguu yangu, hayo tu;
29. kama walivyonifanyia hao wana wa Esau waketio Seiri, na hao Wamoabi waketio Ari; hata nivuke Yordani niingie nchi tupewayo na BWANA, Mungu wetu.
30. Lakini Sihoni mfalme wa Heshboni hakutuacha kupitia kwake; kwa kuwa BWANA, Mungu wako, alimfanya mgumu roho yake, akamtia ukaidi moyoni mwake, apate mtia mkononi mwako kama alivyo hivi leo.
31. Kisha BWANA akaniambia, Tazama, nimeanza kumtoa Sihoni na nchi yake mbele yako; anza kuimiliki, upate kuirithi nchi yake.
32. Ndipo Sihoni alipotutokea juu yetu yeye na watu wake wote, kupigana huko Yahasa.
33. BWANA, Mungu wetu, akamtoa mbele yetu, tukampiga yeye na wanawe, na watu wake wote.
34. Tukatwaa miji yake yote wakati huo, tukaharibu kabisa kila mji uliokuwa na watu, pamoja na wanawake na wadogo; tusimsaze hata mmoja;