Kum. 19:11-20 Swahili Union Version (SUV)

11. Lakini mtu awaye yote akimchukia mwenziwe na kumwotea na kumwinukia, akampiga hata akafa; naye akakimbilia miji hii mmojawapo;

12. ndipo wazee wa mji wake wapeleke ujumbe kumtwaa huko, na kumuua katika mkono wa mwenye kulipiza kisasi cha damu, apate kufa.

13. Jicho lako lisimhurumie, lakini uondoe damu ya asiye makosa katika Israeli, ili upate kufanikiwa.

14. Usiiondoe alama ya mpaka wa jirani yako, waliouweka watu wa kale katika urithi wako, utakaorithi ndani ya nchi akupayo BWANA, Mungu wako, uimiliki.

15. Shahidi mmoja asimwinukie mtu awaye yote kumshuhudia kwa uovu wo wote, wala kwa dhambi yo yote, katika makosa akosayo yo yote; jambo na lithibitishwe kwa vinywa vya mashahidi wawili, au watatu.

16. Shahidi mdhalimu akimwinukia mtu ye yote na kushuhudia juu yake ya upotoe;

17. ndipo wale watu washindanao kwa mambo yale na wasimame wote wawili mbele za BWANA, mbele ya makuhani na waamuzi watakaokuwapo siku hizo;

18. nao waamuzi na watafute kwa bidii; na tazama, yule shahidi akiwa shahidi wa uongo, naye ametoa ushahidi wa uongo juu ya nduguye;

19. ndipo mtamfanyia kama alivyodhani kumfanyia nduguye; ndivyo utakavyoondoa uovu katikati yako.

20. Na watakaosalia watasikia na kuogopa, wasifanye tena uovu mfano wa huo katikati yako.

Kum. 19