Kum. 19:1-10 Swahili Union Version (SUV)

1. BWANA, Mungu wako, atakapoyakatilia mbali hayo mataifa yenye nchi akupayo BWANA, Mungu wako, nawe ukawafuata, na kukaa katika miji yao, na katika nyumba zao;

2. itenge miji mitatu iwe kwako katikati ya nchi yako, akupayo BWANA, Mungu wako, kuimiliki.

3. Itengeze njia, igawanye na mipaka ya nchi yako, akurithishayo BWANA, Mungu wako, iwe mafungu matatu, ili kwamba kila mwenye kuua mtu apate kukimbilia huko.

4. Na hii ndiyo hukumu ya mwenye kuua mtu, atakayekimbilia huko awe hai; atakayemwua mwenziwe pasipo kukusudia, wala hakumchukia tangu hapo;

5. kama aingiapo mtu na mwenziwe mwituni kwenda kukata kuni, akapeleka mkono wake na shoka ili kukata mti, likatoka shoka katika mpini, likampiga yule mwenziwe hata akafa; basi na akimbilie katika miji hii mmojawapo awe hai;

6. asije akaandamiwa mwuaji na mwenye kulipiza kisasi cha damu, moyo wake ukali na hasira, akampata kwa njia kuwa ndefu, akamwua; wala hana haki ya kuuawa, kwa kuwa hakumchukia tangu hapo.

7. Kwa sababu hii ninakuamuru, na kukuambia, Ujitengee miji mitatu.

8. Na kama BWANA, Mungu wako, akiueneza mpaka wako kama alivyowaapia baba zako, akakupa na nchi yote aliyoahidi kwamba atawapa baba zako;

9. nawe ukiyashika maagizo haya yote nikuagizayo leo, na kuyafanya, kumpenda BWANA, Mungu wako, na kwenda sikuzote katika njia zake, ndipo ujiongezee miji mitatu tena, pamoja na mitatu ile;

10. isije ikamwagika damu ya asiye makosa kati ya nchi yako akupayo BWANA, Mungu wako, iwe urithi, ikawa na damu juu yako.

Kum. 19