10. Asionekane kwako mtu ampitishaye mwanawe au binti yake kati ya moto, wala asionekane mtu atazamaye bao, wala mtu atazamaye nyakati mbaya, wala mwenye kubashiri, wala msihiri,
11. wala mtu alogaye kwa kupiga mafundo, wala mtu apandishaye pepo, wala mchawi, wala mtu awaombaye wafu.
12. Kwa maana mtu atendaye hayo ni chukizo kwa BWANA; kisha ni kwa sababu ya hayo BWANA, Mungu wako, anawafukuza mbele yako.
13. Uwe mkamilifu kwa BWANA, Mungu wako.
14. Maana mataifa haya utakaowamiliki huwasikiliza wanaoshika nyakati mbaya na kutazama bao; bali wewe, BWANA, Mungu wako, hakukupa ruhusa kutenda hayo.
15. BWANA, Mungu wako, atakuondokeshea nabii miongoni mwa ndugu zako kama nilivyo mimi; msikilizeni yeye.
16. Kama vile ulivyotaka kwa BWANA, Mungu wako, huko Horebu, siku ya kusanyiko, ukisema, Nisisikie tena sauti ya BWANA, Mungu wangu, wala nisiuone tena moto huu mkubwa, nisije nikafa.
17. BWANA akaniambia, Wametenda vema kusema walivyosema.
18. Mimi nitawaondokeshea nabii miongoni mwa ndugu zao mfano wako wewe, nami nitatia maneno yangu kinywani mwake, naye atawaambia yote nitakayomwamuru.
19. Hata itakuwa, mtu asiyesikiliza maneno yangu atakayosema yule kwa jina langu, nitalitaka kwake.
20. Lakini nabii atakayenena neno kwa kujikinai kwa jina langu, ambalo sikumwagiza kulinena, au atakayenena katika jina la miungu mingine, nabii yule atakufa.
21. Nawe ukisema moyoni mwako, Tutajuaje neno asilolinena BWANA?
22. Atakaponena nabii kwa jina la BWANA, lisifuate jambo lile wala kutimia, hilo ndilo neno asilolinena BWANA; kwa kujikinai amelinena huyo nabii, usimwogope