1. Utunze mwezi wa Abibu, ukamfanyie pasaka BWANA, Mungu wako, kwa kuwa ilikuwa ni mwezi wa Abibu alipokutoa Misri usiku BWANA; Mungu wako.
2. Nawe umchinjie pasaka BWANA, Mungu wako, katika kundi la kondoo na la ng’ombe, mahali atakapochagua BWANA apakalishe jina lake.
3. Usimle pamoja na mikate iliyotiwa chachu; siku saba utakula naye mikate isiyotiwa chachu, nayo ni mikate ya mateso; kwa maana ulitoka nchi ya Misri kwa haraka; ili upate kukumbuka siku uliyotoka nchi ya Misri, siku zote za maisha yako.
4. Wala isionekane kwako chachu muda wa siku saba katika mipaka yako yote; wala katika hiyo nyama uchinjayo siku ya kwanza jioni, kisilale cho chote usiku kucha hata asubuhi.
5. Usimchinje pasaka ndani ya malango yako yote akupayo BWANA, Mungu wako;
6. ila mahali atakapochagua BWANA, Mungu wako, apakalishe jina lake, ndipo mtakapomchinja pasaka jioni, katika machweo ya jua, kwa wakati kama uliotoka Misri.
7. Nawe umwoke na kumla mahali atakapochagua BWANA, Mungu wako; kisha asubuhi yake ugeuke uende hemani mwako.