Kum. 13:2-13 Swahili Union Version (SUV)

2. ikatukia hiyo ishara au hiyo ajabu aliyokuambia akisema, Na tuifuate miungu mingine usiyoijua, tuitumikie hiyo;

3. wewe usiyasikize maneno ya nabii yule, au yule mwotaji wa ndoto, kwa kuwa BWANA, Mungu wenu, yuawajaribu, apate kujua kwamba mwampenda BWANA, Mungu wenu, kwa mioyo yenu yote na roho zenu zote.

4. Tembeeni kwa kumfuata BWANA, Mungu wenu; mcheni na kushika maagizo yake na kuisikia sauti yake, nanyi mtumikieni na kushikamana naye.

5. Na yule nabii, au yule mwotaji wa ndoto, na auawe, kwa kuwa amesema yaliyopotoka juu ya BWANA, Mungu wenu, aliyewatoa katika nchi ya Misri, akakukomboa katika nyumba ya utumwa, apate yule mtu kukupotoa katika njia aliyokuamuru BWANA, Mungu wako, uiendee. Ndivyo utakavyouondoa uovu utoke katikati yako.

6. Atakapokushawishi kwa siri ndugu yako, mwana wa mamaako, au mwana wako, au binti yako, au mke wa kifuani mwako, au rafiki yako aliye kama moyo wako, akikuambia, Twende tukaabudu miungu mingine usiyoijua wewe wala baba zako;

7. katika miungu ya mataifa yaliyo kando-kando yenu karibu nawe au mbali nawe, tokea ncha moja ya dunia hata ncha ya pili ya dunia;

8. usimkubalie wala usimsikize; wala jicho lako lisimwonee huruma, wala usimwache, wala usimfiche;

9. mwue kweli; mkono wako na uwe wa kwanza juu yake katika kumwua, na baadaye mikono ya watu wote.

10. Nawe mtupie mawe hata afe; kwa kuwa alitaka kukupotoa na BWANA, Mungu wako aliyekutoa katika nchi ya Misri, katika nyumba ya utumwa.

11. Na Israeli wote watasikia na kuogopa, wasifanye tena uovu mfano wa huo katikati yako.

12. Ukisikia yasemwa habari ya miji yako mmojawapo, akupayo BWANA, Mungu wako, ukae humo, ukiambiwa,

13. Kumetoka katikati yako mabaradhuli kadha wa kadha, wamewapotoa wenyeji wa mji wao, wakisema, Twendeni tukaabudu miungu mingine msiyoijua;

Kum. 13