Kum. 12:15-25 Swahili Union Version (SUV)

15. Pamoja na haya waweza kuchinja nyama na kula ndani ya malango yako yote, kwa kufuata yote yatamaniwayo na roho yako, kwa mfano wa baraka ya BWANA, Mungu wako, aliyokupa; aliye tohara na asiye tohara ana ruhusa kula katika nyama hiyo, kama ya paa na ya kulungu.

16. Lakini msiile damu; imwageni juu ya nchi kama maji.

17. Usile ndani ya malango yako zaka ya nafaka zako, wala ya divai yako, wala ya mafuta yako, wala wazaliwa wa kwanza wa makundi yako, ya ng’ombe wala ya kondoo, wala nadhiri zako uwekazo zo zote, wala sadaka zako za hiari, wala sadaka ya kuinuliwa ya mkono wako;

18. lakini hivyo mtakula mbele za BWANA, Mungu wako, mahali atakapochagua BWANA, Mungu wako, wewe, na mwanao mume na mke, na mtumwa wako mume na mke, na Mlawi aliye ndani ya malango yako; nawe furahi mbele za BWANA, Mungu wako, katika yote utakayotia mkono wako.

19. Jilinde nafsi yako usimwache Mlawi siku zote uishizo katika nchi yako.

20. BWANA, Mungu wako, atakapoongeza mpaka wako, kama alivyokuahidi, nawe utakaposema, Nataka kula nyama, kwa kuwa roho yako yatamani kula nyama; waweza kula nyama, kwa kufuata yote inayotamani roho yako.

21. Na mahali atakapochagua BWANA, Mungu wako, apaweke jina lake, pakiwa mbali nawe mno, ndipo utakapochinja katika kundi lako la ng’ombe na kondoo alilokupa BWANA kama nilivyokuagiza, nawe utakula ndani ya malango yako, kwa kufuata yote inayotamani roho yako.

22. Kama vile aliwavyo paa na kulungu, ndivyo utakavyoila nyama hii; asiyekuwa tohara na aliye tohara wataila pia.

23. Ila ujihadhari kwamba usile damu, kwani ile damu ndiyo uhai; na uhai usile pamoja na nyama.

24. Usiile; imwage juu ya nchi kama maji.

25. Usiile; ili upate kufanikiwa, na watoto wako baada yako utakapofanya yaliyoelekea machoni pa BWANA.

Kum. 12