11. lakini nchi mwivukiayo kuimiliki ni nchi ya vilima na mabonde, nayo hunyweshwa maji ya mvua ya mbinguni;
12. nayo ni nchi itunzwayo na BWANA, Mungu wako; macho ya BWANA Mungu wako, ya juu yake, tangu mwanzo wa mwaka hata mwisho wa mwaka.
13. Tena itakuwa, mtakaposikiza kwa bidii maagizo yangu niwaagizayo leo, kwa kumpenda BWANA, Mungu wenu, na kumtumikia kwa mioyo yenu yote na roho zenu zote,
14. ndipo nitakapowapa mvua ya nchi yenu kwa wakati wake, mvua ya masika, na mvua ya vuli, upate kuvuna nafaka yako, na divai yako, na mafuta yako.
15. Nami nitakupa nyasi katika mavue yako kulisha wanyama wako wa mifugo, nawe utakula na kushiba.
16. Jitunzeni nafsi zenu, mioyo yenu isije ikadanganywa, mkageuka na kutumikia miungu mingine na kuiabudu;
17. hasira za BWANA zikawaka juu yenu, naye akafunga mbingu kusiwe na mvua, wala nchi isitoe matunda yake; mkaangamia kwa upesi mtoke katika nchi nzuri awapayo BWANA.
18. Kwa hiyo yawekeni maneno yangu mioyoni mwenu na rohoni mwenu; yafungeni yawe dalili juu ya mikono yenu, nayo yatakuwa kama utepe katikati ya macho yenu.
19. Nayo wafunzeni vijana vyenu kwa kuyazungumza uketipo katika nyumba yako, na utembeapo njiani, na ulalapo, na uondokapo.
20. Tena yaandike juu ya miimo ya nyumba yako, na juu ya malango yako;
21. ili siku zenu zifanywe nyingi, na za vijana vyenu nao, juu ya nchi BWANA aliyowaapia baba zenu kuwa atawapa, kama zilivyo siku za mbingu juu ya nchi.
22. Kwa kuwa kwamba mtayashika kwa bidii maagizo haya yote niwaagizayo, kuyafanya; kumpenda BWANA, Mungu wenu, na kutembea katika njia zake zote, na kushikamana naye;
23. ndipo BWANA atakapowafukuza mataifa haya yote mbele yenu, nanyi mtamiliki mataifa makubwa yenye nguvu kuwapita ninyi.