1. Ninyi akina bwana, wapeni watumwa wenu yaliyo haki na ya adili, mkijua ya kuwa ninyi nanyi mna Bwana mbinguni.
2. Dumuni sana katika kuomba, mkikesha katika kuomba huku na shukrani;
3. mkituombea na sisi pia, kwamba Mungu atufungulie mlango kwa lile neno lake, tuinene siri ya Kristo, ambayo kwa ajili yake nimefungwa,
4. ili niidhihirishe, kama inipasavyo kunena.
5. Enendeni kwa hekima mbele yao walio nje, mkiukomboa wakati.
6. Maneno yenu yawe na neema siku zote, yakikolea munyu, mpate kujua jinsi iwapasavyo kumjibu kila mtu.
7. Tikiko, ndugu mpendwa, mtumishi mwaminifu, mjoli wangu katika Bwana, atawaarifu mambo yangu yote;
8. ambaye nimemtuma kwenu kwa sababu iyo hiyo, ili mjue mambo yetu, naye akawafariji mioyo yenu;