Kol. 3:16-25 Swahili Union Version (SUV)

16. Neno la Kristo na likae kwa wingi ndani yenu katika hekima yote, mkifundishana na kuonyana kwa zaburi, na nyimbo, na tenzi za rohoni; huku mkimwimbia Mungu kwa neema mioyoni mwenu.

17. Na kila mfanyalo, kwa neno au kwa tendo, fanyeni yote katika jina la Bwana Yesu, mkimshukuru Mungu Baba kwa yeye.

18. Ninyi wake, watiini waume zenu, kama ipendezavyo katika Bwana.

19. Ninyi waume, wapendeni wake zenu msiwe na uchungu nao.

20. Ninyi watoto, watiini wazazi wenu katika mambo yote; maana jambo hili lapendeza katika Bwana.

21. Ninyi akina baba, msiwachokoze watoto wenu, wasije wakakata tamaa.

22. Ninyi watumwa, watiini hao ambao kwa mwili ni bwana zenu, katika mambo yote, si kwa utumwa wa macho, kama wajipendekezao kwa wanadamu, bali kwa unyofu wa moyo, mkimcha Bwana.

23. Lo lote mfanyalo, lifanyeni kwa moyo, kama kwa Bwana, wala si kwa wanadamu,

24. mkijua ya kuwa mtapokea kwa Bwana ujira wa urithi. Mnamtumikia Bwana Kristo.

25. Maana adhulumuye atapata mapato ya udhalimu wake, wala hakuna upendeleo.

Kol. 3