7. Bwana MUNGU asema hivi, Neno hili halitasimama wala halitakuwa.
8. Kwa maana kichwa cha Shamu ni Dameski, na kichwa cha Dameski ni Resini; na katika muda wa miaka sitini na mitano Efraimu atavunjika vipande vipande, asiwe kabila ya watu tena;
9. tena kichwa cha Efraimu ni Samaria, na kichwa cha Samaria ni mwana wa Remalia. Kwamba hamtaki kusadiki, bila shaka hamtathibitika.
10. Tena BWANA akasema na Ahazi akinena,
11. Jitakie ishara ya BWANA, Mungu wako; itake katika mahali palipo chini sana, au katika mahali palipo juu sana.
12. Lakini Ahazi akasema, Sitaitaka, wala sitamjaribu BWANA.
13. Naye akasema, Sikilizeni sasa, enyi nyumba ya Daudi; Je! Ni neno dogo kwenu kuwachosha wanadamu, hata mkataka kumchosha Mungu wangu pia?
14. Kwa hiyo Bwana mwenyewe atawapa ishara. Tazama, bikira atachukua mimba, atazaa mtoto mwanamume, naye atamwita jina lake Imanueli.
15. Siagi na asali atakula, wakati ajuapo kuyakataa mabaya na kuyachagua mema.