1. Hata ikawa katika siku za Ahazi, mwana wa Yothamu, mwana wa Uzia, mfalme wa Yuda, Resini, mfalme wa Shamu, na Peka, mwana wa Remalia, mfalme wa Israeli, wakapanda wakaenda Yerusalemu ili kupigana nao, lakini hawakuweza kuushinda.
2. Kisha watu wa nyumba ya Daudi wakaambiwa kwamba Shamu wamefanya mapatano na Efraimu. Na moyo wake ukataharuki, na moyo wa watu wake, kama miti ya mwituni itikiswavyo na upepo.
3. Basi BWANA akamwambia Isaya, Haya, toka, umlaki Ahazi, wewe na Shear-yashubu mwana wako, huko mwisho wa mfereji wa birika la juu, katika njia kuu ya uwanja wa dobi;
4. ukamwambie, Angalia, ukatulie; usiogope wala usife moyo, kwa sababu ya mikia hii miwili ya vinga hivi vitokavyo moshi; kwa sababu ya hasira kali ya Resini na Shamu, na mwana wa Remalia.
5. Kwa kuwa Shamu amekusudia mabaya juu yako, pamoja na Efraimu na mwana wa Remalia, wakisema,
6. Haya, na tupande ili kupigana na Yuda na kuwasumbua, tukabomoe mahali tupate kuingia, na kummilikisha mfalme ndani yake, huyo mwana wa Tabeeli.
7. Bwana MUNGU asema hivi, Neno hili halitasimama wala halitakuwa.
8. Kwa maana kichwa cha Shamu ni Dameski, na kichwa cha Dameski ni Resini; na katika muda wa miaka sitini na mitano Efraimu atavunjika vipande vipande, asiwe kabila ya watu tena;
9. tena kichwa cha Efraimu ni Samaria, na kichwa cha Samaria ni mwana wa Remalia. Kwamba hamtaki kusadiki, bila shaka hamtathibitika.
10. Tena BWANA akasema na Ahazi akinena,
11. Jitakie ishara ya BWANA, Mungu wako; itake katika mahali palipo chini sana, au katika mahali palipo juu sana.
12. Lakini Ahazi akasema, Sitaitaka, wala sitamjaribu BWANA.