1. BWANA asema hivi, Mbingu ni kiti changu cha enzi, na dunia ni mahali pa kuweka miguu yangu; mtanijengea nyumba ya namna gani? Na mahali pangu pa kupumzikia ni mahali gani?
2. Maana mkono wangu ndio uliofanya hivi vyote, vitu hivi vyote vikapata kutokea, asema BWANA; lakini mtu huyu ndiye nitakayemwangalia, mtu aliye mnyonge, mwenye roho iliyopondeka, atetemekaye asikiapo neno langu.
3. Yeye achinjaye ng’ombe ni kama yeye amwuaye mtu; na yeye atoaye dhabihu ya mwana-kondoo ni kama yeye avunjaye shingo ya mbwa; na yeye atoaye matoleo ni kama yeye atoaye damu ya nguruwe; na yeye afukizaye uvumba ni kama yeye abarikiye sanamu; naam, wamezichagua njia zao wenyewe, na nafsi zao zafurahia machukizo yao.
4. Mimi nami nitachagua mapigo yao, nitaleta hofu zao juu yao; kwa sababu nilipoita, hawakuitika; na niliponena, hawakusikia; bali walifanya yaliyo maovu machoni pangu, na kuyachagua nisiyoyafurahia.
5. Lisikilizeni neno la BWANA, ninyi mtetemekao kwa sababu ya neno lake; Ndugu zenu wawachukiao ninyi, waliowatupa kwa ajili ya jina langu, wamesema, Na atukuzwe BWANA, tupate kuiona furaha yenu; lakini watatahayarika.
6. Sauti ya fujo itokayo mjini!Sauti itokayo hekaluni!Sauti ya BWANA awalipaye adui zake adhabu!
7. Kabla hajaona utungu alizaa;Kabla maumivu yake hayajampata,Alizaa mtoto mwanamume.
8. Ni nani aliyesikia neno kama hili?Ni nani aliyeona mambo kama haya?Je! Nchi yaweza kuzaliwa siku moja?Taifa laweza kuzaliwa mara?Maana Sayuni, mara alipoona utungu,Alizaa watoto wake.
9. Je! Mimi nilete wana karibu na kuzaliwa, nisizalishe? Asema BWANA; mimi nizalishaye, je! Nilifunge tumbo? Asema Mungu wako.