1. Watu wasionitaka wanauliza habari zangu; nimeonekana na hao wasionitafuta; naliliambia taifa lisiloitwa kwa jina langu,
2. Nitazameni, nitazameni. Mchana kutwa nimewanyoshea mikono yangu watu walioasi, watu waendao katika njia isiyo njema, wakifuata mawazo yao wenyewe;
3. watu wanikasirishao mbele za uso wangu daima, wakitoa dhabihu katika bustani zao, na kufukiza uvumba juu ya matofali;
4. waketio kati ya makaburi, na kulala katika mahali pao pa siri; walao nyama ya nguruwe, na mchuzi wa vitu vinichukizavyo u katika vyombo vyao;
5. watu wasemao, Simama peke yako, usinikaribie mimi, kwa maana mimi ni mtakatifu kuliko wewe; watu hao ni moshi puani mwangu, moto uwakao mchana kutwa.
6. Tazama, neno hili limeandikwa mbele zangu. Sitanyamaza, lakini nitalipa, naam, mimi nitawalipa ujira wao vifuani mwao;
7. maovu yenu na maovu ya baba zenu pamoja, asema BWANA, ninyi mliofukiza uvumba juu ya milima, na kunitukana juu ya vilima; basi, kwa ajili ya hayo nitawapimia kwanza kazi yao vifuani mwao.