Isa. 64:1-9 Swahili Union Version (SUV)

1. Laiti ungepasua mbingu, na kushuka, ili milima iteteme mbele zako;

2. kama vile moto uchomapo vichaka, na moto uchemshapo maji; ili kuwajulisha adui zako jina lako, mataifa wakatetemeke mbele zako!

3. Ulipofanya mambo ya kutisha tusiyoyatazamia, ulishuka, milima ikatetema mbele zako.

4. Maana tangu zamani za kale watu hawakusikia, wala kufahamu kwa masikio, wala jicho halikuona Mungu, ila wewe, atendaye mambo kwa ajili yake amngojaye.

5. Wewe wamlaki yeye afurahiaye yaliyo haki na kuyatenda, watu wale wakukumbukao katika njia zako; tazama, ulikuwa na hasira, nasi tulitenda dhambi; tumekuwa katika mambo haya muda mwingi; nasi, je! Tutaokolewa?

6. Kwa maana sisi sote tumekuwa kama mtu aliye mchafu, na matendo yetu yote ya haki yamekuwa kama nguo iliyotiwa unajisi; sisi sote twanyauka kama jani, na maovu yetu yatuondoa, kama upepo uondoavyo.

7. Tena hapana aliitiaye jina lako, ajitahidiye akushike; kwa kuwa umetuficha uso wako, nawe umetukomesha kwa njia ya maovu yetu.

8. Lakini sasa, Ee BWANA, wewe u baba yetu; sisi tu udongo, nawe u mfinyanzi wetu; sisi sote tu kazi ya mikono yako.

9. Ee BWANA, usione hasira nyingi, wala usiukumbuke uovu siku zote; tazama, angalia, twakusihi, sisi sote tu watu wako.

Isa. 64