2. lakini maovu yenu yamewafarikisha ninyi na Mungu wenu, na dhambi zenu zimeuficha uso wake msiuone, hata hataki kusikia.
3. Kwa maana mikono yenu imetiwa unajisi kwa damu, na vidole vyenu vimetiwa unajisi kwa uovu; midomo yenu imenena uongo, ndimi zenu zimenong’ona ubaya.
4. Hapana adaiye kwa haki, wala hapana atetaye kwa kweli; hutumainia ubatili, hunena uongo; hupata mimba ya madhara, na kuzaa uovu.
5. Huangua mayai ya fira, na kusuka wavu wa buibui; yeye alaye mayai yao hufa, na hilo livunjwalo hutoka nyoka.
6. Nyavu zao hazitakuwa mavazi, wala hawatajifunika kwa kazi zao; kazi zao ni kazi za uovu, na vitendo vya udhalimu vimo mikononi mwao.
7. Miguu yao hukimbilia mabaya, nao hufanya haraka kumwaga damu isiyo na hatia; mawazo yao ni mawazo ya uovu; ukiwa na uharibifu zaonekana katika njia kuu zao.
8. Njia ya amani hawaijui; wala hapana hukumu ya haki katika miendo yao; wamejifanyizia njia zilizopotoka; kila apitaye katika njia hizo hajui amani.
9. Kwa sababu hiyo hukumu ya haki i mbali nasi, wala haki haitufikilii; twatazamia nuru, na kumbe! Latokea giza; twatazamia mwanga, lakini twaenda katika giza kuu.
10. Twapapasa-papasa kutafuta ukuta kama kipofu, naam, twapapasa kama watu wasio na macho; twajikwaa wakati wa adhuhuri, kana kwamba ni wakati wa ukungu wa alfajiri; kati yao waliowanda tumekuwa kama wafu.
11. Sisi sote twanguruma kama dubu; twaomboleza kama hua; twatazamia hukumu ya haki, lakini hapana; na wokovu, lakini u mbali nasi.
12. Maana makosa yetu yamezidi kuwa mengi mbele zako, na dhambi zetu zashuhudia juu yetu; maana makosa yetu tunayo pamoja nasi, na maovu yetu tumeyajua;
13. katika kukosa na kumkana BWANA, na katika kugeuka tusimfuate Mungu wetu, tukinena jeuri na uasi, na kukusudia maneno ya uongo na kuyatoa moyoni.
14. Na hukumu imegeuka ikaenda nyuma, na haki inasimama mbali sana; maana kweli imeanguka katika njia kuu, na unyofu hauwezi kuingia.