1. Tazama, mkono wa BWANA haukupunguka, hata usiweze kuokoa wala sikio lake si zito, hata lisiweze kusikia;
2. lakini maovu yenu yamewafarikisha ninyi na Mungu wenu, na dhambi zenu zimeuficha uso wake msiuone, hata hataki kusikia.
3. Kwa maana mikono yenu imetiwa unajisi kwa damu, na vidole vyenu vimetiwa unajisi kwa uovu; midomo yenu imenena uongo, ndimi zenu zimenong’ona ubaya.
4. Hapana adaiye kwa haki, wala hapana atetaye kwa kweli; hutumainia ubatili, hunena uongo; hupata mimba ya madhara, na kuzaa uovu.
5. Huangua mayai ya fira, na kusuka wavu wa buibui; yeye alaye mayai yao hufa, na hilo livunjwalo hutoka nyoka.
6. Nyavu zao hazitakuwa mavazi, wala hawatajifunika kwa kazi zao; kazi zao ni kazi za uovu, na vitendo vya udhalimu vimo mikononi mwao.