Isa. 54:1-10 Swahili Union Version (SUV)

1. Imba, wewe uliye tasa, wewe usiyezaa; paza sauti yako kwa kuimba, piga kelele, wewe usiyekuwa na utungu; maana watoto wake aliyeachwa ni wengi kuliko watoto wake yeye aliyeolewa, asema BWANA.

2. Panua mahali pa hema yako, na wayatandaze mapazia ya maskani yako; usiwakataze; ongeza urefu wa kamba zako; vikaze vigingi vya hema yako.

3. Kwa maana utaenea upande wa kuume na upande wa kushoto; na wazao wako watawamiliki mataifa; wataifanya miji iliyokuwa ukiwa kukaliwa na watu.

4. Usiogope; maana hutatahayarika; wala usifadhaike; maana hutaaibishwa; kwa kuwa utaisahau aibu ya ujana wako, pia mashutumu ya ujane wako hutayakumbuka tena.

5. Kwa sababu Muumba wako ni mume wako; BWANA wa majeshi ndilo jina lake; na Mtakatifu wa Israeli ndiye Mkombozi wako; Yeye ataitwa Mungu wa dunia yote.

6. Maana BWANA amekuita kama mke aliyeachwa na kuhuzunishwa rohoni, kama mke wakati wa ujana, atupwapo, asema Mungu wako.

7. Kwa kitambo kidogo nimekuacha; lakini kwa rehema nyingi nitakukusanya.

8. Kwa ghadhabu ifurikayo nalikuficha uso wangu dakika moja; lakini kwa fadhili za milele nitakurehemu, asema BWANA, Mkombozi wako.

9. Kwa maana jambo hili limekuwa kama maji ya Nuhu kwangu; maana kama nilivyoapa ya kwamba maji ya Nuhu hayatapita juu ya dunia tena, kadhalika nimeapa ya kwamba sitakuonea hasira, wala kukukemea.

10. Maana milima itaondoka, na vilima vitaondolewa; bali wema wangu hautaondoka kwako, wala agano langu la amani halitaondolewa; asema BWANA akurehemuye.

Isa. 54