Isa. 48:8-17 Swahili Union Version (SUV)

8. Naam, hukusikia; naam, hukujua; naam, tokea zamani sikio lako halikuzibuka; maana nalijua ya kuwa wewe watenda kwa hila nyingi, nawe umeitwa mkosaji tangu kuzaliwa kwako;

9. kwa ajili ya jina langu nitaahirisha hasira yangu, na kwa ajili yako nitajizuia, ili nisifiwe, wala nisikukatilie mbali.

10. Tazama, nimekusafisha, lakini si kama fedha; nimekuchagua katika tanuru ya mateso.

11. Kwa ajili ya nafsi yangu, kwa ajili ya nafsi yangu, nitatenda haya; je! Litiwe unajisi jina langu? Wala sitampa mwingine utukufu wangu.

12. Nisikilize mimi, Ee Yakobo; na Israeli, niliyekuita; mimi ndiye. Mimi ni wa kwanza, na mimi ni wa mwisho pia.

13. Naam, mkono wangu umeuweka msingi wa dunia, na mkono wangu wa kuume umezitanda mbingu; niziitapo husimama pamoja.

14. Kusanyikeni, ninyi nyote, mkasikie; ni nani miongoni mwao aliyehubiri haya? BWANA amempenda; atatimiza mapenzi yake juu ya Babeli, na mkono wake utakuwa juu ya Wakaldayo.

15. Mimi, naam, mimi, nimenena; naam, nimemwita; nimemleta, naye ataifanikisha njia yake.

16. Nikaribieni, sikieni haya; tokea mwanzo sikunena kwa siri; tangu yalipokuwapo, mimi nipo; na sasa Bwana MUNGU amenituma, na roho yake.

17. BWANA, mkombozi wako, mtakatifu wa Israeli, asema hivi; Mimi ni BWANA, Mungu wako, nikufundishaye ili upate faida, nikuongozaye kwa njia ikupasayo kuifuata.

Isa. 48