2. Maana hujiita wenyeji wa mji mtakatifu, hujitegemeza juu ya Mungu wa Israeli; BWANA wa majeshi ni jina lake.
3. Mimi nimehubiri mambo ya kale tangu zamani; naam, yalitoka katika kinywa changu, nikayadhihirisha; naliyatenda kwa ghafula, yakatokea.
4. Kwa sababu nalijua ya kuwa wewe u mkaidi, na shingo yako ni shingo ya chuma, na kipaji cha uso wako ni shaba;
5. basi nimekuonyesha tangu zamani; kabla hayajatukia nalikuonyesha; usije ukasema, Sanamu yangu imetenda haya; sanamu yangu ya kuchonga, na sanamu yangu ya kuyeyusha, imeyaamuru.
6. Umesikia haya; tazama haya yote; nanyi, je! Hamtayahubiri? Nimekuonyesha mambo mapya tangu wakati huu, naam, mambo yaliyofichwa, usiyoyajua.
7. Yameumbwa sasa, wala si tokea zamani; na kabla ya siku hii ya leo hukusikia habari yake; usije ukasema, Tazama, naliyajua.