Isa. 48:2-10 Swahili Union Version (SUV)

2. Maana hujiita wenyeji wa mji mtakatifu, hujitegemeza juu ya Mungu wa Israeli; BWANA wa majeshi ni jina lake.

3. Mimi nimehubiri mambo ya kale tangu zamani; naam, yalitoka katika kinywa changu, nikayadhihirisha; naliyatenda kwa ghafula, yakatokea.

4. Kwa sababu nalijua ya kuwa wewe u mkaidi, na shingo yako ni shingo ya chuma, na kipaji cha uso wako ni shaba;

5. basi nimekuonyesha tangu zamani; kabla hayajatukia nalikuonyesha; usije ukasema, Sanamu yangu imetenda haya; sanamu yangu ya kuchonga, na sanamu yangu ya kuyeyusha, imeyaamuru.

6. Umesikia haya; tazama haya yote; nanyi, je! Hamtayahubiri? Nimekuonyesha mambo mapya tangu wakati huu, naam, mambo yaliyofichwa, usiyoyajua.

7. Yameumbwa sasa, wala si tokea zamani; na kabla ya siku hii ya leo hukusikia habari yake; usije ukasema, Tazama, naliyajua.

8. Naam, hukusikia; naam, hukujua; naam, tokea zamani sikio lako halikuzibuka; maana nalijua ya kuwa wewe watenda kwa hila nyingi, nawe umeitwa mkosaji tangu kuzaliwa kwako;

9. kwa ajili ya jina langu nitaahirisha hasira yangu, na kwa ajili yako nitajizuia, ili nisifiwe, wala nisikukatilie mbali.

10. Tazama, nimekusafisha, lakini si kama fedha; nimekuchagua katika tanuru ya mateso.

Isa. 48