13. Naam, mkono wangu umeuweka msingi wa dunia, na mkono wangu wa kuume umezitanda mbingu; niziitapo husimama pamoja.
14. Kusanyikeni, ninyi nyote, mkasikie; ni nani miongoni mwao aliyehubiri haya? BWANA amempenda; atatimiza mapenzi yake juu ya Babeli, na mkono wake utakuwa juu ya Wakaldayo.
15. Mimi, naam, mimi, nimenena; naam, nimemwita; nimemleta, naye ataifanikisha njia yake.
16. Nikaribieni, sikieni haya; tokea mwanzo sikunena kwa siri; tangu yalipokuwapo, mimi nipo; na sasa Bwana MUNGU amenituma, na roho yake.
17. BWANA, mkombozi wako, mtakatifu wa Israeli, asema hivi; Mimi ni BWANA, Mungu wako, nikufundishaye ili upate faida, nikuongozaye kwa njia ikupasayo kuifuata.
18. Laiti ungalisikiliza amri zangu! Ndipo amani yako ingalikuwa kama mto wa maji, na haki yako kama mawimbi ya bahari;
19. Tena wazao wako wangalikuwa kama mchanga, na hao waliotoka katika tumbo lako kama chembe zake; jina lake lisingalikatika, wala kufutwa mbele zangu.
20. Haya, tokeni katika Babeli,Kimbieni kutoka kwa Wakaldayo;Hubirini kwa sauti ya kuimba, tangazeni haya,Yatamkeni mpaka mwisho wa dunia, semeni,BWANA amemkomboa mtumishi wake, Yakobo.
21. Wala hawakuona kiu alipowaongoza jangwani;Alitoa maji katika mwamba kwa ajili yao;Pia akaupasua mwamba, maji yakatoka kwa nguvu.
22. Hapana amani kwa wabaya, asema BWANA.