1. Sikieni haya, enyi watu wa nyumba ya Yakobo, mnaoitwa kwa jina la Israeli, mliotoka katika maji ya Yuda; mnaoapa kwa jina la BWANA, na kumtaja Mungu wa Israeli, lakini si kwa kweli, wala si kwa haki.
2. Maana hujiita wenyeji wa mji mtakatifu, hujitegemeza juu ya Mungu wa Israeli; BWANA wa majeshi ni jina lake.
3. Mimi nimehubiri mambo ya kale tangu zamani; naam, yalitoka katika kinywa changu, nikayadhihirisha; naliyatenda kwa ghafula, yakatokea.
4. Kwa sababu nalijua ya kuwa wewe u mkaidi, na shingo yako ni shingo ya chuma, na kipaji cha uso wako ni shaba;
5. basi nimekuonyesha tangu zamani; kabla hayajatukia nalikuonyesha; usije ukasema, Sanamu yangu imetenda haya; sanamu yangu ya kuchonga, na sanamu yangu ya kuyeyusha, imeyaamuru.
6. Umesikia haya; tazama haya yote; nanyi, je! Hamtayahubiri? Nimekuonyesha mambo mapya tangu wakati huu, naam, mambo yaliyofichwa, usiyoyajua.
7. Yameumbwa sasa, wala si tokea zamani; na kabla ya siku hii ya leo hukusikia habari yake; usije ukasema, Tazama, naliyajua.
8. Naam, hukusikia; naam, hukujua; naam, tokea zamani sikio lako halikuzibuka; maana nalijua ya kuwa wewe watenda kwa hila nyingi, nawe umeitwa mkosaji tangu kuzaliwa kwako;