Isa. 45:7-20 Swahili Union Version (SUV)

7. Mimi naiumba nuru, na kulihuluku giza; mimi nafanya suluhu, na kuhuluku ubaya; Mimi ni BWANA, niyatendaye hayo yote.

8. Dondokeni, enyi mbingu, toka juu,Mawingu na yamwage haki;Nchi na ifunuke, ili kutoa wokovu,Nayo itoe haki ikamee pamoja;Mimi, BWANA, nimeiumba.

9. Ole wake ashindanaye na Muumba wake! Kigae kimoja katika vigae vya dunia! Je! Udongo umwambie yeye aufinyangaye; Unafanya nini? Au kazi yako, Hana mikono?

10. Ole wake amwambiaye baba yake, Wazaa nini? Au mwanamke, Una utungu wa nini?

11. BWANA, Mtakatifu wa Israeli, na Muumba wake, asema hivi; Niulize habari za mambo yatakayokuja; mambo ya wana wangu, na habari ya kazi ya mikono yangu; haya! Niagizeni.

12. Mimi nimeiumba dunia, nimemhuluku mwanadamu juu yake; Mimi, naam, mikono yangu mimi, imezitanda mbingu, na jeshi lake lote nimeliamuru.

13. Mimi nimemwinua katika haki, nami nitazinyosha njia zake zote; ataujenga mji wangu, naye atawaacha huru watu wangu waliohamishwa, si kwa kulipwa fedha, wala kwa kupewa zawadi, asema BWANA wa majeshi.

14. BWANA asema hivi, Kazi ya Misri, na bidhaa ya Kushi, na Waseba, watu walio warefu, watakujilia, nao watakuwa wako; watakufuata; watakuja katika minyororo; wataanguka chini mbele yako, watakuomba, wakisema, Hakika Mungu yu ndani yako; wala hapana mwingine, hapana Mungu tena.

15. Hakika wewe u Mungu ujifichaye nafsi yako, Ee Mungu wa Israeli, Mwokozi.

16. Watatahayarika, naam, watafadhaika, wote pia; wale wafanyao sanamu wataingia fadhaa pamoja.

17. Bali Israeli wataokolewa na BWANA kwa wokovu wa milele; ninyi hamtatahayarika, wala kufadhaika, milele na milele.

18. Maana BWANA, aliyeziumba mbingu, asema hivi; Yeye ni Mungu; ndiye aliyeiumba dunia na kuifanya; ndiye aliyeifanya imara; hakuiumba ukiwa, aliiumba ili ikaliwe na watu; Mimi ni BWANA, wala hapana mwingine.

19. Sikusema kwa siri, katika mahali pa nchi ya giza; sikuwaambia wazao wa Yakobo; Nitafuteni bure; Mimi, BWANA, nasema haki; nanena mambo ya adili.

20. Jikusanyeni mje; na kukaribia pamoja, ninyi wa mataifa mliookoka; hawana maarifa wale wachukuao mti wa sanamu yao ya kuchonga; wamwombao mungu asiyeweza kuokoa.

Isa. 45