Isa. 45:15-21 Swahili Union Version (SUV)

15. Hakika wewe u Mungu ujifichaye nafsi yako, Ee Mungu wa Israeli, Mwokozi.

16. Watatahayarika, naam, watafadhaika, wote pia; wale wafanyao sanamu wataingia fadhaa pamoja.

17. Bali Israeli wataokolewa na BWANA kwa wokovu wa milele; ninyi hamtatahayarika, wala kufadhaika, milele na milele.

18. Maana BWANA, aliyeziumba mbingu, asema hivi; Yeye ni Mungu; ndiye aliyeiumba dunia na kuifanya; ndiye aliyeifanya imara; hakuiumba ukiwa, aliiumba ili ikaliwe na watu; Mimi ni BWANA, wala hapana mwingine.

19. Sikusema kwa siri, katika mahali pa nchi ya giza; sikuwaambia wazao wa Yakobo; Nitafuteni bure; Mimi, BWANA, nasema haki; nanena mambo ya adili.

20. Jikusanyeni mje; na kukaribia pamoja, ninyi wa mataifa mliookoka; hawana maarifa wale wachukuao mti wa sanamu yao ya kuchonga; wamwombao mungu asiyeweza kuokoa.

21. Hubirini, toeni habari; naam, na wafanye mashauri pamoja; ni nani aliyeonyesha haya tangu zamani za kale? Ni nani aliyeyahubiri hapo zamani? Si mimi, BWANA? Wala hapana Mungu zaidi ya mimi; Mungu mwenye haki, mwokozi; hapana mwingine zaidi ya mimi.

Isa. 45