Isa. 42:9-18 Swahili Union Version (SUV)

9. Tazama, mambo ya kwanza yamekuwa, nami nayahubiri mambo mapya; kabla hayajatokea nawapasheni habari zake.

10. Mwimbieni BWANA wimbo mpya,Na sifa zake tokea mwisho wa dunia;Ninyi mshukao baharini, na vyote vilivyomo,Na visiwa, nao wakaao humo.

11. Jangwa na miji yake na ipaze sauti zao,Vijiji vinavyokaliwa na Kedari;Na waimbe wenyeji wa Sela,Wapige kelele toka vilele vya milima.

12. Na wamtukuze BWANA,Na kutangaza sifa zake visiwani.

13. BWANA atatokea kama shujaa;Ataamsha wivu kama mtu wa vita;Atalia, naam, atapiga kelele;Atawatenda adui zake mambo makuu.

14. Siku nyingi nimenyamaza kimya; nimenyamaza, nikajizuia; sasa nitapiga kelele kama mwanamke aliye katika kuzaa; nitaugua na kutweta pamoja.

15. Nitaharibu milima na vilima, nitavikausha vyote vimeavyo; nitaifanya mito ya maji kuwa visiwa, na kuyakausha maziwa ya maji.

16. Nitawaleta vipofu kwa njia wasiyoijua; katika mapito wasiyoyajua nitawaongoza; nitafanya giza kuwa nuru mbele yao; na mahali palipopotoka kuwa pamenyoka. Haya nitayatenda, wala sitawaacha.

17. Watarudishwa nyuma, wataaibishwa sana, hao wanaotumainia sanamu za mawe, na kuziambia sanamu za madini, Ninyi ndinyi miungu yetu.

18. Sikilizeni, enyi viziwi; tazameni, enyi vipofu, mpate kuona.

Isa. 42