12. Na wamtukuze BWANA,Na kutangaza sifa zake visiwani.
13. BWANA atatokea kama shujaa;Ataamsha wivu kama mtu wa vita;Atalia, naam, atapiga kelele;Atawatenda adui zake mambo makuu.
14. Siku nyingi nimenyamaza kimya; nimenyamaza, nikajizuia; sasa nitapiga kelele kama mwanamke aliye katika kuzaa; nitaugua na kutweta pamoja.
15. Nitaharibu milima na vilima, nitavikausha vyote vimeavyo; nitaifanya mito ya maji kuwa visiwa, na kuyakausha maziwa ya maji.
16. Nitawaleta vipofu kwa njia wasiyoijua; katika mapito wasiyoyajua nitawaongoza; nitafanya giza kuwa nuru mbele yao; na mahali palipopotoka kuwa pamenyoka. Haya nitayatenda, wala sitawaacha.
17. Watarudishwa nyuma, wataaibishwa sana, hao wanaotumainia sanamu za mawe, na kuziambia sanamu za madini, Ninyi ndinyi miungu yetu.
18. Sikilizeni, enyi viziwi; tazameni, enyi vipofu, mpate kuona.
19. Ni nani aliye kipofu, ila mtumishi wangu? Au aliye kiziwi, kama mjumbe wangu nimtumaye? Ni nani aliye kipofu, kama yeye aliye na amani? Naam, kipofu kama mtumishi wa BWANA?
20. Unaona mambo mengi, lakini huyatii moyoni; masikio yake ya wazi, lakini hasikii.
21. BWANA akapendezwa, kwa ajili ya haki yake, kuitukuza sheria, na kuiadhimisha.
22. Lakini watu hawa ni watu walioibiwa na kutekwa; wote wamenaswa katika mashimo, wamefichwa katika magereza; wamekuwa mawindo, wala hapana aokoaye; wamekuwa mateka, wala hapana asemaye, Rudisha.
23. Ni nani miongoni mwenu atakayetega sikio lake kuyasikia hayo? Atakayesikiliza na kusikia kwa wakati ujao?