15. Hezekia akamwomba BWANA, akisema,
16. Ee BWANA wa majeshi, Mungu wa Israeli, ukaaye juu ya makerubi, wewe, naam, wewe peke yako, ndiwe Mungu wa falme zote za dunia. Wewe ndiwe uliyeziumba mbingu na nchi.
17. Tega sikio lako, BWANA, usikie; funua macho yako, BWANA, uone; uyasikie maneno ya Senakeribu, aliyopeleka ili kumtukana Mungu aliye hai.
18. Ni kweli, BWANA, wafalme wa Ashuru wameziharibu nchi zote, na mashamba yao,
19. na kuwatupa miungu yao motoni; kwa maana hao hawakuwa miungu, bali kazi ya mikono ya wanadamu; walikuwa miti na mawe, ndiyo sababu wakawaharibu.
20. Basi sasa, BWANA, Mungu wetu, utuokoe na mkono wake, falme zote za dunia zipate kujua ya kuwa wewe ndiwe BWANA, wewe peke yako.
21. Ndipo Isaya, mwana wa Amozi, akapeleka ujumbe kwa Hezekia, akisema, BWANA, Mungu wa Israeli, asema hivi, Kwa kuwa umeniomba juu ya Senakeribu, mfalme wa Ashuru,
22. tamko alilolitamka BWANA katika habari zake ndilo hili; Bikira, binti Sayuni, anakudharau, anakudhihaki sana; binti Yerusalemu anatikisa kichwa chake juu yako.
23. Ni nani uliyemshutumu na kumtukana? Umeinua sauti yako juu ya nani, na kuinua macho yako juu? Juu ya Mtakatifu wa Israeli.