1. Nyika na mahali palipo ukiwa patafurahi; jangwa litashangilia na kuchanua maua kama waridi.
2. Litachanua maua mengi, na kufurahi, naam, kwa shangwe na kuimba; litapewa uzuri wa Lebanoni, utukufu wa Karmeli na Sharoni; watauona utukufu wa BWANA, ukuu wa Mungu wetu.
3. Itieni nguvu mikono iliyo dhaifu, yafanyeni imara magoti yaliyolegea.
4. Waambieni walio na moyo wa hofu, Jipeni moyo, msiogope; tazama, Mungu wenu atakuja na kisasi, na malipo ya Mungu; atakuja na kuwaokoa ninyi.