7. Kwa maana Misri huwasaidia bure, bila faida;Kwa hiyo nimemwita, Rahabu aketiye kimya.
8. Haya, enenda sasa, andika neno hili katika kibao mbele ya macho yao, lichore katika kitabu ili liwe kwa ajili ya majira yatakayokuja, kwa ushuhuda hata milele.
9. Kwa maana watu hawa ni watu waasi, watoto wasemao uongo, watoto wasiotaka kuisikia sheria ya BWANA;
10. wawaambiao waonaji, Msione; na manabii, Msitoe unabii wa mambo ya haki, tuambieni maneno laini, hubirini maneno yadanganyayo;
11. tokeni katika njia, geukeni mtoke katika mapito; mkomesheni Mtakatifu wa Israeli mbele yetu.
12. Basi kwa ajili ya hayo Mtakatifu wa Israeli asema hivi, Kwa sababu mwalidharau neno hili, na kutumainia jeuri na ukaidi, na kuyategemea hayo;
13. basi, uovu huu utakuwa kwenu kama mahali palipobomoka, palipo tayari kuanguka patokezapo katika ukuta mrefu, ambapo kuvunjika kwake huja ghafula kwa mara moja.
14. Naye atapavunja kama chombo cha mfinyanzi kivunjwavyo, akikivunja-vunja asiache kukivunja, hata hakipatikani katika vipande vyake kigae kitoshacho kutwaa moto jikoni, au kuteka maji kisimani.