Isa. 30:1-10 Swahili Union Version (SUV)

1. Ole wa watoto waasi; asema BWANA; watakao mashauri lakini hawayataki kwangu mimi; wajifunikao kifuniko lakini si cha roho yangu; wapate kuongeza dhambi juu ya dhambi;

2. waendao kutelemkia Misri wala hawakuuliza kinywani mwangu; ili wajitie nguvu kwa nguvu za Farao, na kutumainia kivuli cha Misri.

3. Basi, nguvu za Farao zitakuwa aibu yenu, na kutumainia kivuli cha Misri kutakuwa kufadhaika kwenu.

4. Kwa maana wakuu wake wako Soani, na wajumbe wake wamefika Hanesi.

5. Wote watawaonea haya watu wasioweza kuwafaidia, wasio na msaada wala faida, bali ni aibu na sababu ya kushutumiwa.

6. Ufunuo juu ya hayawani wa Negebu.Katikati ya nchi ya taabu na dhiki,Ambayo hutoka huko simba jike na simba,Nyoka na joka la moto arukaye,Huchukua mali zao mabegani mwa punda wachanga,Na hazina zao juu ya nundu za ngamiaWaende kwa watu ambao hawatawafaa kitu.

7. Kwa maana Misri huwasaidia bure, bila faida;Kwa hiyo nimemwita, Rahabu aketiye kimya.

8. Haya, enenda sasa, andika neno hili katika kibao mbele ya macho yao, lichore katika kitabu ili liwe kwa ajili ya majira yatakayokuja, kwa ushuhuda hata milele.

9. Kwa maana watu hawa ni watu waasi, watoto wasemao uongo, watoto wasiotaka kuisikia sheria ya BWANA;

10. wawaambiao waonaji, Msione; na manabii, Msitoe unabii wa mambo ya haki, tuambieni maneno laini, hubirini maneno yadanganyayo;

Isa. 30