Isa. 3:14-26 Swahili Union Version (SUV)

14. BWANA ataingia katika kuwahukumu wazee wa watu wake na wakuu wao; Ninyi ndinyi mliokula shamba la mizabibu; vitu mlivyowateka maskini vi ndani ya nyumba zenu.

15. Ni nini maana yake, ninyi kuwaonea watu wangu, na kuseta nyuso za maskini? Asema Bwana, BWANA wa majeshi.

16. BWANA akasema tena, Kwa sababu binti za Sayuni wana kiburi, na kuenenda na shingo zilizonyoshwa, na macho ya kutamani, wakienenda kwa hatua za madaha, na kuliza njuga kwa miguu yao;

17. Basi, kwa hiyo, Bwana atawapiga binti za Sayuni kwa pele za utosini, na BWANA ataifunua aibu yao.

18. Siku hiyo BWANA atawaondolea uzuri wa njuga zao, na kaya zao;

19. na pete za masikio, na vikuku, na taji zao;

20. na dusumali, na mafurungu, na vitambi, na vibweta vya marashi, na matalasimu;

21. na pete, na azama,

22. na mavazi ya sikukuu, na debwani; na shali, na vifuko;

23. na vioo vidogo, na kitani nzuri, na vilemba, na utaji.

24. Hata itakuwa ya kuwa badala ya manukato mazuri kutakuwa uvundo, na badala ya mishipi, kamba; na badala ya nywele zilizosukwa vizuri, upaa; na badala ya kisibau, mavazi ya kigunia; na kutiwa alama mwilini kwa moto badala ya uzuri.

25. Watu wako waume wataanguka kwa upanga, na mashujaa wako vitani.

26. Na malango yake yatalia na kuomboleza, naye atakuwa ukiwa, atakaa chini.

Isa. 3