5. Lakini wingi wa adui zako utakuwa kama mavumbi membamba, na wingi wao watishao utakuwa kama makapi yapitayo; naam, itakuwa mara na kwa ghafula.
6. Naye atajiliwa na BWANA wa majeshi kwa ngurumo, na tetemeko la nchi, na sauti kuu, na chamchela, na tufani, na mwali wa moto uteketezao.
7. Na wingi wa mataifa wapiganao na Arieli, wote wapiganao naye na ngome yake, nao wamwudhio, watakuwa kama ndoto, na maono ya usiku.
8. Tena itakuwa kama mtu mwenye njaa aotapo, kumbe, anakula; lakini aamkapo, nafsi yake haina kitu; na kama mtu mwenye kiu aotapo, kumbe, anakunywa; lakini aamkapo, kumbe, anazimia, na nafsi yake inatamani; hivyo ndivyo utakavyokuwa huo wingi wa mataifa waletao vita juu ya mlima Sayuni.
9. Ngojeni mstaajabu; fanyeni anasa zenu na kuwa vipofu; wamelewa wala si kwa mvinyo; wamewaya-waya wala si kwa sababu ya kileo.
10. Kwa maana BWANA amewamwagieni roho ya usingizi, amefumba macho yenu, yaani, manabii; amefunika vichwa vyenu, yaani, waonaji.
11. Na maono yote yamekuwa kwenu kama maneno ya chuo kilichotiwa muhuri, ambacho watu humpa mtu aliye na maarifa, wakisema, Tafadhali ukisome hiki; akasema, Siwezi, kwa kuwa kimetiwa muhuri;
12. kisha chuo hiki apewa mtu asiye na maarifa, akaambiwa, Kisome hicho tafadhali, akasema, Sina maarifa mimi.