Isa. 26:14-21 Swahili Union Version (SUV)

14. Wao wamekufa, hawataishi; wamekwisha kufariki, hawatafufuka; kwa sababu hiyo umewajilia, na kuwaangamiza, na kuupoteza ukumbusho wao.

15. Umeliongeza hilo taifa, BWANA, umeliongeza taifa; wewe umetukuzwa, umeipanua mipaka yote ya nchi hii.

16. BWANA, katika taabu zao walikwenda kwako; waliomba maombi mengi wakati adhabu yako ilipokuwa juu yao.

17. Kama vile mwanamke mwenye mimba anayekaribia wakati wake wa kuzaa, alivyo na utungu na kulia kwa sababu ya maumivu yake, ndivyo tulivyokuwa sisi mbele zako, Ee BWANA.

18. Tumekuwa na mimba, tumekuwa na utungu, tumekuwa kana kwamba tumezaa upepo; hatukufanya wokovu wo wote duniani, wala hawakuanguka wakaao duniani.

19. Wafu wako wataishi, maiti zangu zitafufuka; amkeni, kaimbeni, ninyi mnaokaa mavumbini, kwa maana umande wako ni kama umande wa mimea, nayo ardhi itawatoa waliokufa.

20. Njoni, watu wangu, ingia wewe ndani ya vyumba vyako, ukafunge mlango nyuma yako ujifiche kitambo kidogo, mpaka ghadhabu hii itakapopita.

21. Kwa maana, tazama, BWANA anakuja kutoka mahali pake, ili kuwaadhibu wakaao duniani, kwa sababu ya uovu wao; ardhi nayo itafunua damu yake, wala haitawafunika tena watu wake waliouawa.

Isa. 26