Isa. 22:6-21 Swahili Union Version (SUV)

6. Na Elamu wameshika podo, pamoja na magari ya vita, na watu wenye kupanda farasi; na Kiri wameifunua ngao.

7. Hata ikawa mabonde yako mateule yamejaa magari ya vita, nao wapandao farasi wamejipanga wakielekea malango.

8. Kisha alikiondoa kifuniko cha Yuda, nawe siku hiyo ulivitazama vyombo vya vita katika nyumba ya mwituni.

9. Nanyi mlipaona mahali palipobomoka katika mji wa Daudi ya kuwa ni pengi, nanyi mliyakusanya maji ya birika la chini.

10. Nanyi mlizihesabu nyumba za Yerusalemu, mkazibomoa nyumba ili kuutia nguvu ukuta.

11. Nanyi mlifanya birika la maji katikati ya kuta mbili, la kuwekea maji ya birika la kale; lakini hamkumwangalia yeye aliyeyafanya hayo, wala kumjali yeye aliyeyatengeneza zamani.

12. Siku hiyo Bwana, BWANA wa majeshi, akawaita watu walie na kuomboleza, na kung’oa nywele zao, na kuvaa nguo za magunia;

13. na kumbe! Furaha, na kuchekelea, na kuchinja ng’ombe, na kuchinja kondoo, na kula nyama, na kunywa mvinyo; tule, tunywe, kwa maana kesho tutakufa.

14. Na yeye BWANA wa majeshi akafunua haya masikioni mwangu, Ni kweli, uovu huu hautatakaswa wala kuwatokeni hata mfe; asema Bwana, BWANA wa majeshi.

15. Bwana, BWANA wa majeshi, asema hivi, Haya! Enenda kwa huyu mtunza hazina, yaani, Shebna, aliye juu ya nyumba, ukamwambie,

16. Unafanyaje hapa? Nawe una nani hapa? Hata ukachimba kaburi hapa; ukamchimbia kaburi huko juu, na kumchongea makao katika jabali!

17. Tazama, BWANA atakutupa kwa nguvu, kama mtu mwenye nguvu; naam, atakuzonga-zonga.

18. Hakika atakukunja na kukutupa kama mpira, mpaka nchi iliyo mbali; huko utakufa, na magari ya utukufu wako yatakuwa kuko huko, ewe uliye aibu ya nyumba ya bwana wako.

19. Nami nitakusukuma na kukutoa katika mahali pako, naye atakushusha utoke hapa usimamapo.

20. Na itakuwa katika siku ile nitamwita mtumishi wangu Eliakimu, mwana wa Hilkia;

21. nami nitamvika vazi lako, nitamtia nguvu kwa mshipi wako, nami nitamkabidhi yeye mamlaka yako; naye atakuwa baba kwa wenyeji wa Yerusalemu, na kwa nyumba ya Yuda.

Isa. 22